Aliyekuwa Seneta wa Kakamega Cleophas Malala ameachiliwa huru baada ya kuzuilia katika Kituo cha Polisi cha Eldama Ravine usiku kucha.

Malala alikamatwa Jumatano katika Shule ya Kirobon, Nakuru, ambako alikuwa ameenda kwa mazoezi na klabu ya maigizo ya Butere Girls.

Akihutubia wanahabari kufuatia kuachiliwa kwake, Malala aliwapongeza wanafunzi wa Shule hiyo ya Butere kwa ujasiri wao baada ya kususia kuigiza mchezo wake wa ‘Echoes of War’.

Aidha amemyoshea kidole cha lawama rais William Ruto kufuatia kisa hicho ambacho kimeibua hisia mseto kwenye mitandao ya kijamii.

Wakati huohuo waziri wa elimu nchini Julias Ogamba amekanusha madai kwamba serikali imehusika na kisa cha wanafunzi wa shule ya upili ya wasichana ya Butere kutoigiza mchezo wao wa Echoes of War.

Kwa mujibu wa ogamba ambaye amezungumza na waandishi wa habari ameeleza kuwa wanafunzi hao walikosa kuigiza mchezo wao kwa hiari baada ya kuimba wimbo wa taifa.

Hali kadhalika chama cha ODM na Amnesty International hazijaachwa nyuma katika kuzungumzia suala hili ambapo zimelaani kile walichokitaja kuwa mashambulizi ya kikatili dhidi ya wanafunzi na wanahabari katika Tamasha la Kitaifa la uigizaji na Filamu mjini Nakuru.

Katika taarifa, ODM ilikashifu serikali, ikisisitiza kwamba wasichana hao walipaswa kuruhusiwa kuigiza kama wengine.Chama hicho kilisema kuwa uhuru wa kujieleza unaruhusu Wakenya kujieleza bia uwoga wowote.

Kwa upande wake shirika la Amnesty International lilisema matukio ya Alhamisi asubuhi hayakuwa tu matumizi mabaya ya mamlaka ya polisi lakini shambulio la moja kwa moja kwa uhuru wa kikatiba.

Liliongeza kuwa kwa kulenga mchezo wa shule, serikali inaharamisha ubunifu na kubadilisha maeneo ya kitamaduni kuwa maeneo ya hofu na udhibiti, ikitaka kusitishwa mara moja kwa aina yoyote ya vitisho.

April 10, 2025

Leave a Comment