Ripoti mpya ya Amnesty International imefichua kuwa takriban watu 11 walipoteza maisha katika kaunti za Kisumu na Kisii wakati wa maandamano dhidi ya serikali majuma mawili yaliyopita.
Matokeo kutoka kwa ripoti hiyo, iliyotolewa kwa pamoja na Chama cha mawakili LSK na Chama cha Madaktari Kenya KMA, yanaonyesha kuwa polisi walitumia nguvu kupita kiasi kuwatawanya waandamanaji wakati wa ghasia hizo.
Ripoti hiyo pia ilibainisha kuwa katika kipindi hicho, kesi 107 za shambulio la polisi zilirekodiwa katika kaunti hizo mbili, huku 47 kati ya hizo zikihusiana na risasi.
Kulingana na mashirika hayo, Serikali inapaswa kuhakikisha usalama wa familia na waathiriwa ambao bado hawajaripoti ukiukaji kwa kuhofia vitisho au kudhulumiwa tena katika vituo vya polisi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty International Irungu Houghton tangu wakati huo ameitaka Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) kufanya uchunguzi huru kuhusu visa hivyo vya polisi kuua Wakenya kwa kutumia nguvu kupita kiasi.