Angalau asilimia 75% ya Wakenya wamepinga vikali Mswada wa Fedha wa 2023. Haya ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Kituo cha Masuala ya Fedha CFA kwa ushirikiano na shirika la Twaweza.
Katika uchunguzi wa mtandaoni uliofanywa kati ya Mei 19 na Juni 6, 2023, asilimia 83.8% ya waliohojiwa walionyesha kutoridhishwa kwao na ukosefu wa ushiriki wa wananchi katika kuunda Mswada wa Fedha.
Waliohojiwa pia walipendekeza serikali kushughulikia ufisadi, kupunguza ubadhirifu wa fedha, kupanua wigo wa ushuru kwa kulegeza sheria za ushuru, kulenga vyanzo ambavyo havijatumiwa na kuimarisha usimamizi wa ushuru kama njia za kuinua mapato ya taifa.
Wakenya pia walitoa wito wa kuwepo kwa uwazi ili kusaidia kujenga uaminifu kati ya wananchi na taasisi za serikali. Jumla ya watu 25,966 walihojiwa katika utafiti huo.