Wanafunzi wapatao 1,200 waliokamilisha mtihani wa Gredi ya sita KPSEA pamoja na wale waliofanya mtihani wa darasa la nane wa KCPE katika kaunti ya Narok mwaka jana, bado hawajajiunga na shule wanazofaa hadi kufikia sasa.
Kwa mujibu wa kamishena wa kaunti ya Narok Isaac Masinde, asilimia 94 ya wale wanafunzi ambao walifanya mtihani wao wa gredi ya 6 tayari wamejiunga na shule za upili za ngazi ya chini huku asilimia 93 ya wale ambao walifanya mtihani wao wa KCPE wakiwa tayari wameripoti katika kidato cha kwanza kule Narok.
Akizungumza katika kikao na waandidhi wa habari ofisini mwake mjini Narok, kamishna Masinde amewahimiza machifu sawa na maafisa wengine wanaohusika katika zoezi hili, kukaza kamba ili kuhakikisha kwamba wanafunzi wote wanapata fursa ya kuendeleza masomo yao. Aidha ametoa onyo kali kwa wazazi ambao wanaowazuilia wana wao nyumbani badala ya kuwapeleka shuleni.