Waumini wa kikatoliki katika jimbo Katoliki la Nakuru wamekuwa na siku ya furaha na shangwe, baada ya kutawazwa na kusimikwa kwa Askofu Cleophas Oseso kama askofu mpya wa jimbo hilo.
Hafla ya kutawazwa kwa Askofu Oseso iliandaliwa katika uga wa shule ya upili ya Nakuru, iliongozwa na Mwakilishi papa katika taifa la Kenya na Sudan Kusini Askofu mkuu Hubertus Matheus Maria van Megen, ambaye alimshauri Askofu mpya wa Nakuru kutekeleza wajibu wake kwa njia inayofaa, na kujitolea kwa hali na mali kulitumikia kanisa.
Askofu Cleophas Oseso Tuka alizaliwa tarehe 26 Novemba 1967 eneo la Naivasha, katika dayosisi ya Nakuru. Alisoma falsafa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Augustine huko Mabanga, na theolojia katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Matthias Mulumba ya Tindinyo.
Alitawazwa kuwa kasisi tarehe 24 Juni 1995 katika dayosisi ya Nakuru. Baadaye alitunukiwa shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara kutoka Chuo cha Le Moyne, Marekani, na shahada ya udaktari katika elimu kutoka Wakfu wa Theolojia ya Uzamili, Marekani.
Kabla ya uteuzi wake tarehe 3 Machi 2023, alikuwa akihudumu kama Vicar general wa dayosisi ya Nakuru na paroko wa parokia ya Mtakatifu Augustino huko Bahati, wadhifa aliokuwa akiushikilia tangu 2018.