BY ISAYA BURUGU,31ST MARCH,2023-Balozi wa marekani humu nchini Meg Whitman amelaani kushambuliwa kwa waandishi wa habari katika maandamano yanayofanyika kuipinga serikali nchini humo . Kupitia ujumbe wa Twitter balozi huyo amesema kulinda uhuru wa vyombo vya habari ni msingi wa deomokrasia .
Ujumbe wake huo unajiri baada ya takriban wanahabari sita kujeruhiwa siku ya Alhamisi katika matukio tofauti yaliyowalenga waandishi wa habari na kuwaacha baadhi yao na majeraha mabaya .
Baraza la vyombo vya habari linasema wanahabari 25 wameshambuliwa tangu maandamano hayo kuanza wiki iliyopita.
Katika matukio ya Alhamisi, wanahabari 2 waliripotiwa kupata majeraha kutokana na vitoa machozi vilivyorushwa kwenye gari lao viungani mwa la jijini Nairobi.
Katika video ya kuogofya iliyoshirikiwa na kampuni ya uchunguzi ya Africa Uncensored, mtu aliyejifunika uso akiwa amevalia barakoa ya gesi anakaribia SUV nyeusi. Anaonekana kuvunja moja ya madirisha ya gari hilo kabla ya kurusha bomu la machozi.
Waandishi wawili wa habari wanasemekana kujeruhiwa katika tukio hilo, mmoja akiwa na majeraha makubwa kwenye shavu lake la kulia.
Huko Kisumu, mwanahabari mwingine alijeruhiwa vibaya alipokuwa akirekodi tukio la uporaji.
Taarifa ya Chama cha Wanahabari Kisumu inasema Bw Eric Nabiswa alirushiwa mawe na waporaji waliomwona akiwarekodi na kuanguka na kuvunjika baadhi ya mbavu alipoanguka akijaribu kutoroka.
Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu nchini imelaani ongezeko la mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari wakiwa katika majukumu yao, ikiwa ni pamoja na wizi wa kutumia silaha na kulazimishwa kufuta picha za maandamano na polisi.
Haya yanajiri huku Wadau wa vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari na Chama cha Wahariri nchini , wakiwa wameitisha mkutano wa dharura wikendi hii ili kujadili ongezeko la chuki dhidi ya wanahabari katika machafuko yanayoendelea.