Bunge la Senate jioni ya jana liliidhinisha kuondolewa ofisini kwa aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Meru, Kawira Mwangaza, kwa makosa ya kukiuka katiba, matumizi mabaya ya ofisi, na kutenda kazi bila kuzingatia maadili.
Mswada wa kumwondoa ofisini Gavana Mwangaza uliwasilishwa kwa Bunge la Senate na Spika wa Bunge la Kaunti ya Meru kwa mara ya tatu. Baada ya kuepuka kuondolewa mara mbili zilizopita, hatimaye Mwangaza alipoteza nafasi yake baada ya maseneta kupiga kura ya kuunga mkono mswada huo jana.
Kufuatia uamuzi huo, Mwangaza ameacha rasmi kuhudumu kama Gavana wa Kaunti ya Meru, na nafasi yake sasa itachukuliwa na aliyekuwa Naibu wake Isaac Mutuma M’Ethingia.