Maseneta nchini Kenya wanapanga kuwasilisha mswada mbele ya bunge la taifa lenye lengo la kuzuia magavana waliomaliza mihula yao kushiriki katika siasa mara moja baada ya kumaliza muda wao wa uongozi. Kulingana na mapendekezo hayo, wanasiasa waliohudumu kama magavana hawataruhusiwa kuwania nyadhifa za useneta au wawakilishi wa wadi.
Mapendekezo haya yalijadiliwa siku ya Jumanne katika kikao cha kamati ya seneti kuhusu Haki, Masuala ya Kisheria na Haki za Kibinadamu. Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Bomet Hillary Sigei, inapania kuainisha mapendekezo yao na mswada wa kubadilisha kipengee cha katiba, unaopania kuwazuia wanasiasa waliohudumu kama magavana dhidi ya kuwania wadhifa wowote kwa kipindi cha miaka 5 baada yao kuondoka mamlakani.
Hii ni hatua inayolenga kudumisha uwajibikaji wa viongozi wa serikali za kaunti na kuzuia matumizi mabaya ya nyadhifa za uongozi. Iwapo mswada huo utaidhinishwa na bunge, basi magavana waliohudumu kwa mihula miwili watapata nafasi ya kuwania nyadhifa za ubunge au urais pekee.