Kamati ya Ulinzi na Mahusiano ya Kigeni katika bunge la taifa imeidhinisha uteuzi wa Noordin Haji kuwa Mkurugenzi Mkuu mpya wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS).
Haji ambaye amekuwa akihudumu kama mkurugenzi wa mashtaka ya umma nchini atatwaa kiapo katika kipindi cha siku kadhaa zijazo, kuchukua nafasi ya Philip Kameru ambaye anatazamiwa kustaafu baada ya kushikilia afisi ya NIS tangu Septemba 2014.
Rais William Ruto alimteua Haji kushikilia wadhifa wa NIS, akimrejesha katika ofisi hiyo ambayo aliwahi kuhudumu hapo awali kama Naibu Mkurugenzi wa Kitengo cha Kukabiliana na Uhalifu.
Wakati hayo yakijiri Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Haki na Masuala ya Kisheria (JLAC) pia imeidhinisha uteuzi wa aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Ruto na Caroline Nzilani walioteuliwa katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC).