Chama cha Mameneja wa hifadhi ya Maasai Mara kimejitokeza kukanusha madai kuwa kulikuwa na vifo vya watalii kufuatia mvua kubwa inayoendelea kunyesha na kusababisha mafuriko.
Chama hicho kinasema licha ya mafuriko kusababisha uharibifu wa mali na wanyamapori, watalii wote waliokuwa wakiishi katika maeneo yaliyoathiriwa waliondolewa salama.
Taarifa ya Mwenyekiti wa Chama cha mameneja hao, Harison Nampaso siku ya Jumamosi iliwahakikishia watalii usalama wao kutokana na msimu wa baridi unaoanza Juni.
Kulingana na Chama hicho, maeneo mengi yaliyokumbwa na mafuriko yamefichuliwa kuwa yale yaliyo karibu na Mto Mara, Mto Talek, na Mto Sand ambapo mafuriko yamesababisha watu kuyahama makazi yao, kuharibu kambi na nyumba za kulala za wageni na kuathiri sekta ya utalii na uchumi wa ndani.
Aidha chama hicho kimeiomba serikali kujitokeza na kusaidia ujenzi wa miundombinu muhimu.