BY ISAYA BURUGU,17TH MARCH,2023-Hatimaye wapelelezi wa jinai DCI, kitengo cha kuchunguza visa vya mauaji ya kinyumbani wametoa taarifa iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu kuu na Wakenya kufuatia kifo chenye utata cha kijana Jeff Mwathi aliyefariki nyumbani kwa DJ Fatxo wiki chache zilizopita.

DCI walizamia uchunguzi wa kifo cha kijana huyo baada ya malalamishi mengi kutoka kwa Wakenya ambao walionesha kutoridhishwa kwao na jinsi maafisa wa usalama kutoka kituo cha polisi cha Kasarani walivyokuwa wakiendesha uchunguzi huo.

DCI Ijumaa wiki jana walitangaza kuanzisha uchunguzi dhidi ya kifo cha Jeff, ambaye sehemu ya watu mitandaoni wanahisi huenda alikuwa mwathiriwa wa visa vya ushoga na wengine wakisema kuwa alijiua kwa kujitupa kutoka ghorofa ya 10, katika chumba cha DJ Fatxo mtaani Kasarani.

Mchakato huo ulijumuisha mahojiano ya kundi la kwanza la mashahidi katika kesi hiyo, uchunguzi wa kimahakama wa eneo la tukio na kupatikana kwa picha za CCTV zilizonasa dakika za mwisho za marehemu.

Wataalamu wengine kadhaa wa Uchunguzi wa kina walio katika Maabara ya Kitaifa ya Upelelezi ya DCI ambao wanajumuisha timu ya kushughulikia Mauaji wamekusanya kwa usawa ushahidi muhimu na huo pia unachambuliwa kisayansi

March 17, 2023