Douglas Kanja ambaye amekuwa akihudumu kama kaimu Inspekta jenerali wa polisi kwa majuma mawili, sasa ameteuliwa rasmi kutwaa wadhfa huo ambao uliachwa wazi kufuatia kujiuzulu kwa Japhet Koome baada ya shinikizo kutoka kwa wakenya.
Kupitia taarifa, mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei amesema kuwa Kanja ana vigezo vinavyohitajika kuwa mkuu wa polisi ikizingatiwa kuwa ana uzoefu wa miaka 39 kama afisa wa polisi.
Vilevile Koskei alitangaza kuteuliwa kwa Eliud Kipkoech Langat kama naibu Inspekta jenerali wa polisi huku Gilbert Misengeli akiteuliwa kama naibu inspekta jenerali wa polisi wa utawala.
Aidha kwa sasa Bw. Langat atakaimu wadhfa wa Inspekta jenerali wa polisi huku Kanja akisubiri kupigwa msasa na mabunge yote mawili.