Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Noordin Haji amefutilia mbali mashtaka dhidi ya viongozi sita wa Azimio la umoja, ambayo yalijumuisha maandamano kinyume cha sheria na uharibifu wa mali.
Kupitia kwa wakili wa upande wa mashtaka, DPP alifahamisha mahakama kuwa kuondolewa kwa kesi hizo kutaruhusu kuendelea kwa mazungumzo kati ya serikali na upinzani. Wabunge wa Azimio akiwemo Mbunge wa Ugunja James Opiyo Wandayi, Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo, Mbunge wa Kilifi Kusini Richard Chonga, na Mbunge wa Malindi Amina Mnyazi waliachiliwa huru na Hakimu Mkuu Mwandamizi wa Mahakama ya Kahawa Boaz.
George Yogo Obure na Esther Oromi ambao pia walikuwa washtakiwa pamoja na wabunge hao pia waliachiliwa. Hata hivyo, kesi sawia zinazowakabili waandamanaji 200 katika mahakama za Kibera, Kiambu na Makadara bado zinaendelea.