Mandago

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma ametoa amri ya kukamatwa kwa Seneta wa Kaunti ya Uasin Gishu, Bw. Jackson Mandago, pamoja na washukiwa wengine wawili, kufuatia madai ya kuhusika katika njama ya kuwapunja wanafunzi fedha za masomo ya juu nchini Finland na Canada.

Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini imethibitisha kuanza kwa msako wa seneta huyo ambaye hajulikani alipo tangu jana.Kupitia kwa chapisho kwenye mtandao wa Twitter, Huduma ya Polisi nchini imesema kwamba seneta huyo anatafutwa baada ya kutolewa kwa agizo la kutiwa nguvuni kwake.

https://twitter.com/NPSOfficial_KE/status/1691723925393146163?s=20

Seneta Mandago na washirika wake walichukua fedha za kusaidia kuwapeleka wanafunzi kwa masomo ya Vyuo Vikuu katika mataifa ya Finland na Canada. Baadaye taarifa ziliibuka kuwa gavana huyo amewapunja wazazi na wanafunzi fedha zao baada ya mpango wa kuwapeleka ughaibuni kukosa kutekelezwa.

Huduma ya Kitaifa ya Polisi nchini imeeleza umma kuwa wanamsaka seneta huyo na imetoa wito kwa Bw. Jackson Mandago kujisalimisha kwenye kituo chochote cha polisi. Pia, wananchi wametakiwa kutoa taarifa zozote wanazozijua zinazoweza kusaidia katika kukamatwa kwa seneta huyo.

 

 

August 16, 2023