Renson Mulele Ingonga sasa ndiye mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya Umma (DPP), baada yake kuapishwa asubuhi ya leo kutwaa wadhifa huu rasmi, katika hafla iliyoandaliwa kwenye ikulu ya Nairobi na kushuhudiwa na Rais William Ruto pamoja na wakuu wengine wa serikali na idara ya haki.
Mulele ambaye aliidhinishwa na bunge kufuatia uteuzi wake, ametwaa mikoba ya ofisi hii kutoka kwa Noordin Haji, ambaye anaongoza idara ya ujasusi nchini (NIS). Kabla ya uteuzi wake, alikuwa akihudumu kama naibu wa mkurugenzi wa mashtaka nchini, na sasa anaanza muhula wake wa miaka 8, akiwa anakabiliwa na kibarua cha kurejesha uhuru wa ofisi hiyo ambayo kwa muda imekuwa ikikabiliwa na shutuma za kutumika kisiasa.
Rais william Ruto amemtaka mkurugenzi mpya wa mashtaka ya Umma, kuwa mtetezi wa haki ya wakenya wote, na kumshinikiza kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa katiba. Kauli ya rais imeungwa mkono na rais wa mahakama ya upeo nchini Jaji Mkuu Martha Koome, ambaye ameeleza umuhimu wa ushirikiano ili kufanikisha shughuli zake.