Eneo la Magharibi mwa Kenya linaongoza kwa unywaji wa pombe haramu nchini kote pamoja na pombe za kitamaduni.
Haya ni kwa mujibu wa utafiti mpya wa Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni Dhidi ya Matumizi Mabaya ya Pombe na Madawa ya Kulevya NACADA unaonyesha.
Ripoti iliyotolewa mwezi uliopita inaonyesha kuwa matumizi ya chang’aa yameenea zaidi Magharibi kwa asilimia 11.4, ikifuatiwa na Nyanza kwa asilimia 6.3 na eneo la Bonde la Ufa 3.6.
Na huku Kaunti ya Nairobi ikiongoza kwa unywaji wa pombe iliyotengenezwa kisheria, eneo la Kati linashika nafasi ya pili katika kitengo hicho, likiangazia unywaji pombe kupita kiasi katika eneo lenye watu wengi zaidi nchini Kenya.
NACADA pia ilichunguza kuenea kwa matumizi ya sasa ya aina moja ya mihadarati ambapo eneo la Magharibi pia liliibuka kuwa linaongoza kwa asilimia 26.4 huku mikoa ya Mashariki na Nairobi zikifuata kwa asilimia 20.7 na 19.2 mtawalia.
Kwa ujumla nchini Kenya, pombe ilipatikana kuwa dawa inayotumiwa vibaya zaidi ambapo watu Zaidi ya milioni 3.1 wameathirika ikifuatiwa na Tumbaku na miraa ambazo zinatumiwa na watu Zaidi ya milioni 2.3 na watu 964,737 mtawalia.
Wakati huo huo matumizi mabaya ya bangi yanaathiri watu 518,807 huku dawa zikiathiri watu 60,407 kote nchini.