Enzi ya mtihani wa kitaifa wa darasa la nane KCPE, ilifungwa Rasmi hii leo mwendo wa saa nne na dakika arubaini na tano baada ya watahiniwa wa mwisho wa KCPE kumaliza mtihani wa mwisho wa somo la jamii na dini.
Zaidi ya watahiniwa milioni 1.4 kote nchini waliingia katika vitabu vya kumbukumbu, Kwa kuwa wanafunzi walioanza safari ya mwisho ya mfumo wa elimu wa 8-4-4 ambao umekuwa ukitumika humu nchini kwa miaka 38, tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 1985.
Kikomo rasmi cha mtaala huu, kitakujia mwaka wa 2027, pale wanafunzi waliomaliza KCPE hii leo watakapofanya mtihani wa kidato cha nne wa KCSE. Kulingana na katibu wa elimu ya msingi Belio Kipsang, matokeo ya mitihani ya KCPE na KPSEA iliyokamilika hii leo yatatangazwa kabla ya sherehe za Krismasi.
Wakati huohuo asasi za usalama katika kaunti ndogo ya Narok Kusini zilifanikiwa pakubwa katika kuhakikisha mazingira mazuri yenye usalama wakati wa kipindi cha mitihani ya kitaifa ya KCPE na KPSEA.
Naibu kamishna wa kaunti ya Narok Kusini Felix Kisalu alieleza kwamba ni wakati wa wazazi sasa kuukumbatia kikamilifu mtaala mpya wa masomo unaotegemea umahiri almaarufu CBC.