Familia na jamii katika kaunti hii ya Narok ziko tayari kunufaika kutokana na mpango wa kukabili mabadiliko ya tabianchi.
Mpango huo unalenga kuimarisha uwezo wa jamii kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya hali ya hewa, hasa ukame wa muda mrefu ambao umeathiri familia mingi katika kaunti hii.
Ili kufanikisha mpango huu, mradi wa Sh.177 milioni ulizinduliwa na utatekelezwa na World Vision kwa ushirikiano na serikali ya Narok kupitia ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Ushirikiano wa Korea (KOICA).
Mradi huu umepewa jina la Mazingira Endelevu na Uchumi dhidi ya Ukame na Uharibifu katika Mfumo wa Ikolojia na Usambazaji wa Tsavo.
Mradi huu vilevile unalenga kuwezesha jamii na mbinu za kilimo zinazozingatia hali ya hewa na zinazolenga kuongeza mapato ya kaunti na usalama wa chakula bila kuharibu mazingira.
Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu alisema kuwa mpango huo mpya unaangazia uwezo wa ushirikiano katika kubadilisha jamii katika kaunti hii.