Kidato cha Kwanza Masai Girls High School Narok

Maelfu ya wanafunzi waliokamilisha masomo ya shule ya msingi mwaka jana, wamemiminika katika Shule mbalimbali za upili nchini, ili kujiunga na kidato cha kwanza.

Milolongo mirefu ya wanafunzi pamoja na wazazi wao imeshuhudiwa kuanzia asubuhi ya leo, zaidi ya wanafunzi milioni 1.4 waliokamilisha mtihani wa KCPE wa mwisho chini ya mtaala wa 8-4-4 wakianza maisha mapya kwenye shule za upili.

Shule mojawapo iliyoshuhudia hali hii ni Shule ya Upili ya wasichana ya Maasai Girls mjini Narok. Laini ndefu ya wazazi imeshudiwa kwenye mazingira ya shule hiyo kuanzia asubuhi. Mwalimu Mkuu wa shule, Bi. Cecilia Teeka, amethibitisha kwamba shule hiyo inakusudia kuwapokea wanafunzi wapatao 500, baada ya wizara ya elimu kutoa nafasi 470 kwa wanafunzi kwenye shule hiyo.

Bi. Teeka ameeleza kuwa idadi ya wanafunzi imekuwa ikiongezeka kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, hali inayotokana na matokeo mazuri ya shule hiyo katika mitihani ya kitaifa. Kwa mfano, katika matokeo ya mtihani wa KCSE mwaka jana, wanafunzi 96 walifanikiwa kujihakikishia nafasi za moja kwa moja kwenye vyuo vikuu, ikilinganishwa na wanafunzi 28 waliofuzu mwaka wa 2022.

 

 

January 15, 2024