Gavana wa Kaunti ya Kirinyaga Anne Waiguru amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Magavana kuhudumu kwa muhula wa pili. Waiguru alichaguliwa kwa muhula wa pili afisini kupitia makubaliano ya jumla wakati wa mkutano wa baraza hilo uliofanyika Nairobi.

Wakati huo huo, Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi pia alichaguliwa tena kama Makamu Mwenyekiti wa baraza hilo huku Stephen Sang wa Nandi akipata wadhifa wa mnadhimu. Waiguru alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama Mwenyekiti wa baraza hilo mnamo Septemba 2022.

Kufuatia kuchaguliwa kwake tena, Waiguru alisema kwamba lengo lake sasa litakuwa kuhakikisha kuwa kazi zote zilizogatuliwa na rasilimali zinazofuata zimekabidhiwa kikamilifu kwa serikali za kaunti.

Aliahidi kuangazia kuongeza mgao wa mapato kwa kaunti, kusaidia kaunti kuboresha mapato ya vyanzo vyake na utekelezaji mzuri wa Huduma ya Afya kwa Wote (UHC), ukuzaji wa minyororo ya thamani ya kilimo, uongezaji thamani na biashara.

Waiguru aliwashukuru magavana kwa kuwa na imani na uongozi wake na akaahidi kuelekeza COG kufikia viwango vya juu zaidi.

Mwenyekiti huyo alisema kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita, baraza hilo  limepata mafanikio makubwa zaidi ikiwa ni utoaji wa mgao sawa wa mapato kwa baraza  hasa mwaka 2022/2023 unaolipwa hadi mwisho wa mwaka wa fedha.

Alisema pia kumeimarika mahusiano baina ya serikali kati ya Serikali ya Kitaifa na Kaunti kwa mashauriano na mazungumzo, mengine hadharani.

Hata hivyo, Waiguru alibainisha kuwa muhula wake wa kwanza kama mwenyekiti wa baraza hilo haukukosa changamoto miongoni mwao majaribio ya mara kwa mara ya kurudisha nyuma Ugatuzi kupitia “sheria za kurejesha nyuma na kuunda mashirika yasiyo ya kikatiba kutekeleza majukumu ya ugatuzi.”

October 2, 2023