Ntutu Kina mama Narok

Gavana wa Kaunti ya Narok, Patrick Ntutu, ametoa wito kwa kina mama katika jamii ya Maa kuchukua jukumu kubwa katika kulinda watoto na hasa wale wa kike dhidi ya mimba na ndoa za mapema, hususan wakati huu wa likizo ndefu.

Akizungumza wakati wa ziara yake kwenye Manyatta ya Orkiteng Mugie eneo la Rotian siku ya Alhamisi, Gavana Ntutu ametoa wito kwa wazazi kuhakikisha wanafunzi wanapata mwongozo mzuri wa kupambana na vitendo vya ukeketaji, mimba, na ndoa za mapema, huku akisisitiza umuhimu wa kulinda hadhi ya mtoto wa kike. Vile vile ameeleza umuhimu wa ushirikiano wa kina mama na wanajamii wote katika kukabiliana na changamoto hii inayoshuhudiwa kwa kiasi kikubwa katika kaunti ya Narok.

Aidha, Gavana Ntutu amewataka Moran wa jamii ya Maa kujiepusha na vitendo vya wizi wa mifugo na badala yake kujifunza mienendo ya tamaduni zao za asili. Amesema kwamba elimu na utamaduni wa jamii ya Maa inaweza kuchangia katika kuijenga jamii imara na yenye maendeleo.

Kwa upande wake, Mbunge wa Narok Kaskazini Agnes Pareyio ambaye pia alihudhuria hafla hiyo, amethibitisha kuwa serikali inaweka mikakati madhubuti ya kuthamini mipaka ya msitu wa Mau. Mbunge huyo ameahidi ushirikiano wa karibu na Gavana Ntutu kuhakikisha kwamba hatua za kutosha zinachukuliwa ili kuhifadhi msitu huo muhimu.

 

November 23, 2023