Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja amezungumza kuhusu vita vyake vinavyoendelea na Naibu Rais Rigathi Gachagua kuhusu mipango ya kuondoa matatu kutoka mjini.
Viongozi hao wawili wamepinga maswala hayo huku Sakaja akishikilia kwamba anaungwa mkono kikamilifu na Rais William Ruto kurejesha kile anachokiita hadhi uliopotea wa jiji hilo kwa kuhamisha vituo vya magari ya utumishi wa umma.
Siku ya Jumapili, naibu rais aliwataka wahudumu wa matatu na wafanyabiashara wa jiji la Nairobi kumpuuza Sakaja na kuendelea na biashara zao, akiwahakikishia ulinzi wa serikali dhidi ya mpango anaodai kuwa utakandamiza uchumi wa Nairobi.
Hata hivyo, Sakaja amesema hayuko kwenye vita na Gachagua, akiongeza kuwa naibu rais anastahili kujadili suala hilo naye badala ya kuiongelea kwenye mikutano.