El Niño

Idara ya Mazingira katika Serikali ya Kaunti ya Nairobi imechukua hatua muhimu katika kuhakikisha usafi na usalama wa jiji hilo wakati wa mvua ya El Niño, inayotarajiwa katika maeneo mbalimbali ya taifa.

Hatua hii inajumuisha kuajiri vijana wapatao 3500 ambao watachangia katika juhudi za kudumisha usafi wa jiji, hususan kwa kusafisha njia za maji zilizozibwa.Vijana hawa waliochaguliwa kwa kazi hii waliteuliwa kutoka kwa zaidi ya vijana 65,000 waliotuma maombi yao ya kazi, watashiriki katika kazi ya kudumisha usafi wa jiji ili kuzuia majanga yanayoweza kutokea kutokana na uchafu wakati wa mvua ya El Niño.

Akizungumza wakati wa hafla ya kutangaza mipango ya kukabiliana na athari za mvua ya El Niño jijini Nairobi, Gavana Johnson Sakaja alitoa onyo kwa wale wote wanaojaribu kuhitilafiana na mipango hii ya usalama. Gavana Sakaja alisisitiza kuwa serikali ya kaunti inashirikiana kwa karibu na idara ya utabiri wa hali ya anga ili kuzuia na kupunguza athari za mvua ya El Niño.

Hatua nyingine zilizowekwa na serikali ya kaunti katika kipindi hiki cha maandalizi ni utoaji wa mafunzo kuhusu dharura kwa wananchi wa jiji kuu.

 

September 11, 2023