Maafisa wa polisi wameeleza utayari wao wa kuhakikisha usalama na pia kukabiliana na maandamano yaliyoratibiwa kuandaliwa siku ya Alhamisi. Maandamano hayo yamepewa jina la Nane Nane.
Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Gilbert Masengeli, alisema haya baada ya kuongoza kikao cha maafisa wakuu wa usalama siku ya Jumanne. Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao hicho, alisisitiza kwamba serikali iko macho kuhakikisha haki za Wakenya wote zinaheshimiwa. Hata hivyo, aliwaonya wale wanaotumia maandamano haya kutekeleza vitendo vya uhalifu kwamba watakabiliwa vikali na sheria.
Vijana wa Gen Z wametangaza kuwa watashiriki katika maandamano hayo ya kupinga uongozi mbaya, wakiendeleza juhudi zilizoanza mwezi Juni. Maandamano hayo yalianza kama harakati za kupinga Mswada wa Fedha wa mwaka 2024, ambao baadaye ulitupiliwa mbali. Maandamano hayo aidha yalishuhudia baraza la mawaziri likivunjwa kabla ya Rais kuteua mawaziri wapya, ambao sasa wanatarajiwa kuidhinishwa na bunge.
ACTING IG MASENGELI MEETS WITH REGIONAL AND FORMATION POLICE COMMANDERS
Acting Inspector General- National Police Service Mr. Gilbert Masengeli has asked Police Officers to “uphold teamwork, multi-agency strategy, and professionalism” in their work. pic.twitter.com/CiV959nUqT
— National Police Service-Kenya (@NPSOfficial_KE) August 6, 2024
Kuhusiana na suala la baadhi ya maafisa wa usalama kuvalia mavazi ya raia wakati wa maandamano, Masengeli alisema kwamba maafisa hao wamekubalika kisheria, lakini wanafaa kuwa na nyaraka zinazohitajika kwa ajili ya kujitambulisha kwa wakati wote. Idara ya Huduma za Polisi inatarajiwa kutoa maelezo zaidi na mwongozo wa usalama kabla ya maandamano hayo.