Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amekosoa kauli ya waziri wa viwanda na uwekezaji Moses Kuria, kuhusu uamuzi wa kutochapisha matangazo ya serikali katika gazeti la Daily Nation.
Gachagua aliyezungumza katika kaunti ya Mombasa katika kongamano la kimataifa kuhusu maji na usafi wa Mazingira, alieleza kwamba serikali ya Kenya inaheshimu demokrasia na haitajihusisha na maswala ya ukandamizaji wa vyombo vya habari. Naibu rais hata hivyo aliendelea kusuta vyombo vya habari vinavyoegemea mirengo ya kisiasa, akisema kwamba hatachoka kuwasuta kwa kuenda kinyume na mwongozo wa maadili ya taaluma yao.
Kauli ya Gachagua imejiri saa kadhaa baada ya waziri Moses Kuria kuchapisha kauli za dhihaka katika mitandao yake ya kijamii kuelekea kwa kampuni hiyo ya gazeti. Aidha mashirika mbalimbali pia yammejitokeza na kulaani kauli za waziri huyo.