Jaji mkuu nchini Martha Koome amevunja kimya chake kufuatia kauli ya viongozi wa serikali dhidi ya mahakama. Katika notisi iliyochapishwa kwa wafanyakazi wa idara ya mahakama, jaji Koome amewataka wafanyakazi wote wa mahakama kutoyumbishwa na yeyote katika kazi yao, na kuwataka kuendelea kufuata sheria inavyofaa.

Bi Koome vilevile amelaani matamshi ya kiongozi wa taifa, akiyataja kama yanayoweza kuhitilafiana na kesi zinazoendelea mahakamani. Aidha amemtaka Rais kuwasilisha malalamishi kuhusu ufisadi wa majaji kwenye tume ya JSC ili hatua mwafaka ziweze kuchukuliwa.

Wakati hayo yakijiri, chama cha wanasheria nchini LSK kimemkashifu kiongozi wa Taifa Rais William Ruto, sawa na viongozi wengine serikalini kwa matamshi yao dhidi ya idara za mahakama. Katika taarifa iliyochapishwa na Rais wa LSK Eric Theuri, chama hicho kimemkosoa Rais kwa kutaka kuhitilafiana na utendakazi wa idara huru, badala ya kuwa mtetezi wa kwanza wa sheria nchini.

LSK aidha imetangaza kwamba itaandaa maandamano juma lijalo, ili kuonyesha kutoridhishwa kwao na kauli za rais.

Katika hotuba yake kwenye ibada ya Mazishi huko Nyandarua hapo jana, Kiongozi wa Taifa aliisuta idara ya mahakama kwa kuhitilafiana na kusitisha miradi ya serikali hasa baada ya kupiga breki mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu na ule wa bima mpya ya Afya.

January 3, 2024