Rais William Ruto amefichua kuwa atazindua mradi wa mikopo na akiba wa Hustler Fund tarehe 1 Desemba 2022.Katika hotuba yake kwa taifa wakati wa maadhimisho ya sherehe za 59 za mashujaa, rais aliweka bayana kuwa maswali mengi yameulizwa kuhusu ahadi ya Hustler Fund ambayo likua moja wapo ya ajenda kuu wakati wa kampeni zake kabla ya uchaguzi.
Mpango wa Hustler Fund, unatarajiwa kutoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo kama vile wauzaji wa reja reja, Wafanyikazi wa bodaboda kwenye majukwaa ya kidijitali kwa ada ya chini, na pia kuwafaidi kwa watu binafsi na kupitia vyama, vikundi, saccos na vyama vya ushirika. Aidha rais Ruto alisema kuwa wote watakaofaidi katika mpango huu pia watashiriki katika mpango wa uwekaji wa akiba wa muda mfupi na mpango wa pensheni ambao ni wa muda mrefu.
Katika hotuba hiyo rais aliutaja mpango wa utoaji mikopo kama kichocheo kikubwa cha ukuaji na maendeleo ya taifa, akisisitiza kujitolea kwa serikali ili kuhakikisha kuwa wakenya wanapata mikopo kwa ada inayowaruhusu kulipa mikopo yao na pia kufanya hivo kwa wakati unaofaa na pia bila matatizo yoyote kama yaliyoshuhudiwa hapo awali.
MIPANGO TAYARI IMEANZA
Hata kabla ya kuanza kutekelezwa kwa mpango wa Hustler Fund, rais ameweka wazi kuwa amepata kuafikiana na kampuni ya mawasiliano ya Safaricom ili kushusha ada za mikopo ya Fuliza ambayo imekua ikitegemewa na wakenya wengi katika kujiendeleza kimaisha.
Mengine yaliyoguziwa katika hotuba ya rais ni pamoja na mpango wa kupunguza idadi ya wakenya kutoka katika orodha ya CRB ambayo hujumuisha orodha ya wakenya ambao hawajaweza kulipa deni lao. Rais amesema kuwa hakuna mkenya yeyote atakayeachwa nje ya mikopo hii ili kumpa nafasi ya kujiendeleza.
Rais alipendekeza mpango wa kuwaorodhesha watoro wa deni kwa kuwapa viwango tofauti vya mikopo badala ya kuwafungia nje kabisa, jambo ambalo amesema anatarajia litaanza kutekelezwa hivi karibuni baada ya wakenya wapatao milioni nne kuondolewa katika orodha ya watoro wa deni au CRB.
Kuanza kwa mpango wa Hustler Fund kunatarajiwa kuwa mwanzo wa kuanza kutimizwa kwa ahadi za serikali ya Kenya kwanza ilizotoa kwa wakenya wakati wa Kampeni.