Idadi ya watu waliofariki kufuatia ajali mbaya iliyotokea Idadi ya watu waliofariki kufuatia ajali Ijumaa jioni imeongezeka na kufikia 52 huku watu 32 wakilazwa hospitalini.
Ajali hiyo ya saa kumi na mbili unusu jioni ilitokea baada ya lori kupoteza mwelekeo na kuwagonga wapiti njia, wafanyabiashara na matatu zilizokuwa zimeegeshwa kando ya barabara.
Lori hilo liligonga matatu nne, lori mbili, gari la kibinafsi na basi.
Wakati huohuo waziri wa Barabara na Uchukuzi Kipchumba Murkomen sasa ameagiza kusimamishwa kwa vizuizi vya mwendo kasi katika makutano ya Londiani kaunti ya Kericho kama sehemu ya hatua za kukabiliana na ajali za barabarani.
Akizungumza baada ya kuzuru eneo la tukio leo asubuhi, Murkomen alisema serikali pia itatoa msaada kwa familia za waathiriwa wa ajali hiyo.
Seneta wa Kericho Aaron Cheruyiot kwa upande wake alitoa wito kwa serikali kufungua rasmi hospitali ya Kaunti Ndogo ya Londiani, akitaja ukosefu wa vituo vya afya vya kutosha.
Alisema kuwa vituo vingi vya Kericho vilizidiwa huku waathiriwa wa ajali hiyo wakikimbizwa katika hospitali mbalimbali nchini.