Idara ya Upelelezi wa Jinai DCI imetoa picha za washukiwa wanaodaiwa kuhusika na fujo na ghasia zilizoshuhudiwa siku ya Jumatatu wakati wa maandamano ya kuipinga serikali yakiongozwa na muungano wa upinzani wa Azimio, na kuongeza kuwa msako unaendelea kuwatafuta watu hao.

Kupitia mtandao wa twitter, DCI imetoa msururu wa picha zikiwafichua watu inaowataja kuwa wahalifu waliotumia fursa ya maandamano kuharibu mali na kuwashambulia wananchi wasio na hatia na maafisa wa polisi waliokuwa kazini.

Kulingana na DCI, wakati wa maandamano ya Jumatatu yaliyoongozwa na kiongozi wa chama cha Azimio Raila Odinga, mali ya thamani isiyojulikana yaliharibiwa huku jumla ya maafisa 33 wakiuguza majeraha tofauti na wamelazwa hospitalini.

Aidha  DCI imewataka wananchi kujitolea habari zinazoweza kupelekea kukamatwa kwa washukiwa hao.

March 24, 2023