Idara ya Watoto katika Kaunti ya Narok imetoa wito kwa serikali ya kaunti kuhakikisha kwamba vituo vya kuwatunza watoto wadogo wakati wa mchana, maarufu kama DayCare, vimesajiliwa na vinakidhi viwango vya kisheria.
Hatua hii inalenga kuhakikisha usalama na ulinzi wa watoto, baada ya kutokea visa 3 vya watoto wanaopelekwa kwenye vituo hivyo na kuachwa na wazazi wao.
Pilot Khaemba, afisa wa Idara ya Watoto kaunti ya Narok, amethibitisha kuwa visa hivyo viliripotiwa katika miezi ya Novemba na Disemba mwaka jana. Kulingana na Khaemba, kusajili vituo vya DayCare ni hatua muhimu katika kudhibiti na kuzuia matukio kama hayo yasiweze kujitokeza tena.
Wale wasimamizi wa hivyo vituo (Daycare) wamekuja kwa ofisi wakiripoti kwamba walipokea watoto, na wale watoto, na wale watoto wazazi wao hawajawai kuwakujia”
Bw. Pilot Khaemba, Afisa wa Idara ya watoto katika kaunti ya Narok
Afisa huyo ameongeza kuwa wamiliki wa vituo hivyo wamekuwa na changamoto katika kupata taarifa za watoto waliotelekezwa, kwani wazazi wanaowaleta mara nyingi hawapeani taarifa au nyaraka muhimu zinazohusu watoto hao. Idara hiyo ya Watoto inasisitiza umuhimu wa kuweka mfumo madhubuti wa usajili na ufuatiliaji ili kuhakikisha kuwa watoto wanapokelewa na kuhudumiwa kwa mujibu wa sheria na viwango vilivyowekwa.