Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) inatarajiwa kuwa tayari kufikia Mei mwaka huu, kulingana na jopo la uteuzi wa makamishna wa tume hiyo linaloongozwa na Dkt. Nelson Makanda. Jopo hilo limepokea zaidi ya maombi 300 kutoka kwa Wakenya wanaotaka kushikilia nyadhifa hizo muhimu.
Akizungumza mjini Naivasha, ambapo jopo hilo limekuwa likikutana, naibu mwenyekiti wa jopo la uteuzi Lindah Kilome alihakikishia umma kuwa mchakato wa kuwapiga msasa wagombea utafanywa kwa haki, uwazi, na bila mapendeleo.
Baada ya kukamilika kwa mchujo na mahojiano, jopo litawasilisha majina ya wagombea waliohitimu kwa Rais William Ruto kwa uteuzi. Rais atateua mwenyekiti mmoja na makamishna sita wa tume hiyo.
SOMA PIA | Wanachama wa kamati ya kuwateua makamishna wa IEBC waapishwa.
Ndani ya siku saba baada ya uteuzi wa Rais, majina hayo yatawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kuidhinishwa kabla ya kuteuliwa rasmi. Jopo hilo lilipewa jukumu la kuunda IEBC kwa siku 85 kuanzia tarehe 27 mwezi Januari 2025.