Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome hii leo aliwapandisha kighafla vyeo maafisa wawili wa polisi baada ya kukagua gwaride katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi cha Kiganjo Kaunti ya Nyeri.
Inspekta jenerali ametangaza kuwapandisha maafisa hao hadi ngazi ya Corporal kwa kigezo cha muda waliohudumu katika idara ya polisi. Kisheria hata hivyo, uteuzi huu huenda ukakumbwa na vuta nikuvute, hasa ikizingatiwa kwamba jukumu la kuwapandisha vyeo maafisa wa polisi liko chini ya Tume ya kitaifa ya huduma za polisi(NPSC).
Katika siku za hivi karibuni, Inspeka jenerali amekuwa akikabiliwa na shutuma kutoka kwa idara mbalimbali nchini, kutokana na kuwapandisha vyeo mara kwa mara maafisa wa polisi.
Mwezi juni mwaka huu Tume ya NPSC ilibatilisha agizo la inspekta jenerali la kuwapandisha vyeo zaidi ya maafisa 500 wa polisi.