Jaji Fatuma Sichale Aapishwa Kuiwakilisha Mahakama ya Rufaa katika Tume ya JSC.

Jaji Fatuma Sichale wa Mahakama ya Rufaa ameapishwa kuwa mwakilishi wa mahakama hiyo katika Tume ya Huduma za Mahakama (JSC). Hafla hiyo ya kuapishwa iliandaliwa katika majengo ya mahakama ya upeo nchini na kuhudhuriwa na viongozi wakuu wa mahakama nchini.

Jaji huyo amechukua nafasi hii kufuatia kumalizika kwa mihula miwili ya Jaji Mohammed Warsame, aliyehudumu kwenye wadhifa huo kwa kipindi cha miaka 10. Jaji Warsame ameondoka baada ya kutoa mchango wake thabiti katika kuleta mabadiliko na kusimamia masuala ya haki katika nchini.

Akiongoza hafla hiyo, Jaji Mkuu Martha Koome amempongeza Jaji Sichale kwa uteuzi huo na kumtia moyo kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia uwajibikaji na utaalamu. Jaji Koome ameonyesha imani yake kuwa Jaji Sichale atachangia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha na kuimarisha haki na sheria nchini.

Katika hotuba yake, Jaji Sichale ameiahidi jamii na idara ya mahakama kwamba atatekeleza majukumu yake kwa uwazi na umakinifu mkubwa. Ametoa shukrani zake kwa uongozi uliopita na kwa Jaji Warsame kwa kazi nzuri iliyofanywa katika kipindi chake.

SOMA PIA: Ombi la Kumwondoa Jaji Mkuu Martha Koome Ofisini Lawasilishwa kwa JSC.

Uteuzi wa Jaji Sichale unajiri wakati JSC ina matarajio makubwa kwake katika kusimamia na kuhakikisha uwajibikaji wa hali ya juu katika idara ya mahakama.

 

February 5, 2024