Jaji mkuu Martha Koome amesema kuwa shuguli za mahakama hazitasitishwa kuanzia tarehe 19-21 mwezi huu kama ilivyotangazwa jana na baadhi ya maafisa wa idara ya mahakama.

Kupitia taarifa, Koome ameeleza kuwa mahakama ya makadara tu ndio itasalia kufungwa kufutia ujenzi ambao unaendelea katika mahakama hiyo.

Ameongeza kuwa katika siku zijazo, huduma za mahakama hazitatolewa tena kwa miundo misingi ya muda kama vile hema.

Wakati huohuo, Inspekta Jenerali wa Polisi Japhet Koome amewahakikishia maafisa wote wa mahakama usalama wao wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao kufuatia mauaji ya Hakimu Mkuu wa Mahakama ya Makadara Monica Kivuti.

Katika taarifa yake siku ya Jumatatu, IG Koome alisisitiza kwamba Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) itasalia imara katika kuhakikisha kwamba maafisa wote wa mahakama akiwemo Jaji Mkuu Martha Koome wanapewa usalama wa kudumu.

Usalama wa maafisa wa mahakama uliimarishwa mnamo 2021 wakati Kitengo cha Polisi cha Mahakama kilipoanzishwa ili kutoa usalama kwa Mahakama na kuruhusu ufanisi katika kupata wafanyikazi wa Mahakama.

Koome pia aliifariji familia ya Kivuti kwa kufariki kwake, na kuwatakia afueni ya haraka maafisa wawili waliojeruhiwa wakati wa tukio hilo.

June 17, 2024