Aliyekuwa Mkuu wa majeshi humu nchini Marehemu Jenerali Francis Ogolla, ambaye alifariki katika ajali ya ndege katika kaunti ya Elgeiyo Marakwet, atazikwa Jumapili ya tarehe 21 mwezi wa Aprili nyumbani kwake katika eneo la Alego Usonga, Kaunti ya Siaya.
Kulingana na taarifa iliyochapishwa na Bwana Joel Rabuku Ogolla ambaye ni msemaji wa familia ya jenerali Ogolla, Mkuu huyo wa majeshi aliandika kwenye wosia wake kwamba angependa kuzikwa katika kipindi cha chini ya saa 72 baada ya kifo chake.
SOMA PIA: Luteni Jenerali Francis Omondi Ogolla ateuliwa kuwa Mkuu mpya wa Majeshi.
Familia yake imesema kwamba tayari mipango ya mazishi imeanza na itasimamiwa na serikali kwani Marehemu Jenerali Ogolla aliaga dunia akiwa bado afisini. Ibada ya Wafu inatarajiwa kufuata mazishi hayo, na itaandaliwa Ijumaa ya tarehe 26 mwezi huu katika uwanja wa Ulinzi Sports Complex eneo la Lang’ata.
Kikosi cha Uchunguzi Chawasili Eneo la Ajali ya Ndege ya KDF
Mapema leo Kikosi cha maafisa wa uchunguzi kutoka idara ya Jeshi kiliwasili katika eneo la ajali ya ndege ya KDF siku ya Alhamisi katika eneo la Marakwet Mashariki, kaunti ya Elgeiyo Marakwet. Katika taarifa yake kwa taifa, Rais William Ruto alieleza kuwa Jeshi la Wanahewa limeunda kikosi cha uchunguzi kuchunguza sababu za ajali hiyo ya ndege.