Serikali ya Ethiopia imedai kwamba jeshi la nchi hiyo linadhibiti asilimia 70 ya jimbo la Tigray na kuweka wazi kuwa msaada unatumwa kwenda kwenye eneo hilo.
Taarifa hiyo imetolewa na mshauri wa usalama wa taifa wa Ethiopia Redwan Hussein aliyesema kwamba magari yaliyobeba chakula na dawa yanaelekea kwenye mji wa kimkakati wa Shire na kuwa ndege zinaruhusiwa kutua kwenye eneo hilo.
Hata hivyo madai hayo yamekanushwa vikali na viongozi wa chama cha ukombozi wa umma wa Tigray TPLF waliosema taarifa za serikali hazina ukweli. Taarifa hizo zimekanushwa pia na mfanyakazi wa huduma ya kiutu kwenye jimbo la Tigray ambaye ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hakuna msaada ulioingia jimboni humo hadi sasa. Upelekaji msaada kwenye jimbo la Tigray ni miongoni mwa makubaliano yaliyoafikiwa kati ya serikali na wapiganaji wa TPLF chini ya mkataba wa amani uliotiwa saini baada ya mazungumzo nchini Afrika Kusini.