joto kali kuendelea nchini

Vipindi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya taifa juma hili, kulingana na taarifa kutoka Idara ya Utabiri wa Hali ya Anga nchini. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa joto litazidi kupanda na kufikia viwango vya juu zaidi ya nyuzijoto 30 katika sehemu nyingi za nchi.

Katika baadhi ya maeneo, hali joto linatarajiwa kufikia vipimo vya zaidi ya nyuzijoto 36 wakati wa mchana. Maeneo yaliyotajwa kuathiriwa zaidi na hali hii ni pamoja na kaunti za Turkana, Samburu, Marsabit, Mandera, Wajir, Isiolo, Garissa, Tana River, Lamu, Kilifi, Mombasa, Kwale, Taita Taveta, Kajiado, Makueni, Kitui, Machakos, Nairobi, Kiambu, Embu, Laikipia, Baringo, Elgeyo-Marakwet, West Pokot, Bungoma, Kakamega, Kisumu, Busia, na Narok.

Joto kali limekuwa likishuhudiwa nchini kwa kipindi cha wiki kadhaa sasa, huku wananchi wakishauriwa kuchukua tahadhari zinazofaa ili kujikinga na athari zake. Wataalam wa masuala ya hali ya anga, wameeleza kuwa huenda ongezeko hili la joto limetokana na unyevu ulioongezeka kwenye hewa kutokana na mvua inayonyesha katika baadhi ya maeneo nchini. Aidha baadhi wameeleza kwamba hali hii ambayo hushuhudiwa kila mwaka, imetokana na mzunguko wa jua.

 

February 20, 2024