Kiongozi wa taifa rais William Ruto, ametoa wito kwa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuunga mkono azma ya kinara wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga, katika kugombea nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Muungano wa Afrika (AU)
Akilihutubia Bunge la Afrika Mashariki (EALA) wakati wa ufunguzi rasmi wa kikao cha 5 cha Bunge hilo , kilichofanyika katika majengo ya Bunge jijini Nairobi siku ya Jumanne, rais Ruto ameeleza kwamba viongozi wa mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wameafikiana kwa pamoja kumuunga mkono Odinga katika kampeni yake ya kumrithi Moussa Faki.
Bunge hilo lenye wabunge 63 litakuwa kikao cha wiki tatu zijazo, kikiwa na ajenda mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupokea ripoti za kamati tofauti zinazoshughulikia masuala mbalimbali, chini ya uongozi wa Spika wa EALA, Joseph Ntakirutimana.
Katika hotuba yake vilevile, kiongozi wa taifa amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, akieleza kuwa ukanda huu umeshuhudia maendeleo makubwa na unaelekea kufikia malengo yake ya maendeleo.