Takriban watumizi milioni 11 wa kadi za simu nchini wako katika hatari ywa kufungiwa laini zao, baada ya kukamilika kwa muda uliotolewa kwa watumizi wa kadi hizi kuzisajili upya siku ya Jumamosi 15.10.2022.
Mamlaka ya mawasiliano nchini (CAK) iliagiza wahudumu wa mitandao ya mawasiliano kuwasajili upya wateja wao, kama mojawapo ya njia za kukabiliana na ulaghai unaotekelezwa kupitia laini za simu. Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na kampuni za mawasiliano kuhusu idadi ya waliosajili laini zao, kampuni ya Safaricom inaongoza kwa idadi ya waliosajiliwa ikifanikiwa kusajili laini milioni 38 hii ikiwa ni asilimia 91 ya laini zote zinazotumika chini ya mtandao huo kufikia mwisho mwa Alhamisi 13.10.2022. Kampuni ya mawasiliano ya Airtel imefanikiwa kusajili laini za simu milioni 13.4 ikiwa ni kiwango cha asilimia 78 huku Telkom ikifanikiwa kusajili idadi ya chini zaidi kwa asilimia 40 baada ya kusajili laini milioni 1.8 kufikia jioni yaAlhamisi 13.10.2022.