Rais wa Rwanda Paul Kagame amemtuhumu mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi kwa kutumia migogoro ya mashariki mwa DRC kama kisingizio cha kuchelewesha uchaguzi.
Akizungumza bungeni jana jioni, Kagame alisema dunia nzima inailaumu Rwanda kwa migogoro hiyo, wakati Tshisekedi akijinufaisha kwayo kisiasa.
Kagame amesema ukosefu wa usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaweza kupatiwa ufumbuzi ikiwa nchi moja inayojiandaa kwa uchaguzi mwaka ujao haitautumia kama kisingizio cha hali ya dharura ili kuahirisha uchaguzi wa Kongo unaotarajiwa Disemba mwakani.
Mapigano kati ya jeshi la Kongo na waasi wa M23 yamezidisha mvutano baina ya Kinshasa na Kigali, huku Kongo ikiituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi hao, tuhuma ambazo Rwanda imekuwa ikizikanusha.
Wakati huo huo mazungumzo yanaendelea mjini Nairobi kati ya serikali ya Kongo na makundi ya waasi, katika juhudi za kikanda za kutafuta ufumbuzi wa machafuko mashariki mwa Kongo.