Mawaziri wateule

Kamati ya uteuzi katika Bunge la Taifa imeidhinisha uteuzi wa mawaziri wateule Geoffrey Ruku na Hanna Cheptumo baada ya kufanyiwa mahojiano siku ya Jumatatu. Wawili hao waliteuliwa na Rais katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mwezi uliopita, mabadiliko ambayo pia yalishuhudia kuondolewa kwa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu, Justin Muturi.

Kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge la Taifa Moses Wetang’ula, ilieleza kuwa Ruku na Cheptumo walionyesha weledi na uwezo mkubwa wa kushughulikia majukumu ya wizara zao. Ripoti ya kamati hiyo iliwasilishwa bungeni siku ya Jumanne 15.04.2025 na inatarajiwa kujadiliwa na wabunge hii leo kabla ya uteuzi huo kuidhinishwa rasmi na Bunge.

Waziri mteule wa jinsia, Hanna Cheptumo, aliibua mjadala mkali wakati wa kikao cha kumhoji, baada ya kueleza kuwa ongezeko la mauaji ya wanawake nchini linahusishwa na baadhi ya wasichana wa vyuo vikuu kujiingiza katika shughuli za kutafuta fedha kwenye maeneo ya burudani. Kauli hiyo imezua hisia tofauti mitandaoni huku baadhi ya watu wakimsuta kuhusu maoni yake.

April 16, 2025

Leave a Comment