Kamati ya fedha na Mipango katika bunge la kitaifa, imeidhinisha uteuzi wa Dkt Susan Jemutai Koech kama naibu gavana wa pili wa Benki Kuu nchini (CBK)
Dkt. Jemutai ambaye aliwahi kuhudumu kama katibu mkuu katika wizara ya jumuia ya Afrika Mashariki, alikuwa miongoni mwa watu waliohusishwa pakubwa na Sakata ya ubadhirifu wa fedha za ujenzi wa Mabwawa ya Arror na Kimwarer kabla ya kugeuka shahidi wa upande wa mashtaka.
Mwezi uliopita, Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula alitangaza uteuzi wa Dkt. Koech katika wadhifa huo, kabla ya kamati husika kutwaa jukumu la kupiga msasa ili kumuidhinisha.
Wanachama wa kamati hiyo walikubaliana kwamba Dkt. Koech amehitimu kutwaa wajibu wake kama naibu wa gavana wa benki kuu nchini.