Kamati ya Bunge ya Kitaifa ya Haki na Masuala ya Kisheria imependekeza kuundwa kwa jopo la kuwasikiliza Makamishna wanne wa IEBC wanaochunguzwa.
Makamishna hao wanatuhumiwa kwa ukiukaji mkubwa wa katiba, uzembe na utovu wa nidhamu wakati wa uchaguzi wa Agosti 9.
Kamati hiyo inayoongozwa na mwenyekiti George Murugara pia ilipendekeza Rais William Ruto kuwasimamisha kazi makamishna hao wanne wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Wanne hao ni pamoja na naibu Mwenyekiti Juliana Cherera, Justus Nyang’aya, Francis Wanderi na Irine Masit ambao walitofautiana na mwenyekiti wao Wafula Chebukati kuhusu matokeo ya kura za urais na kukataa matokeo ya mwisho.
Bunge linajadili ripoti hiyo ili kupitishwa jinsi ilivyo au kukataliwa kabisa. Iwapo itapitishwa, basi Rais Ruto anaweza kuwasimamisha kazi wanne hao kesho.