Kamishna wa Kaunti ya Narok, Kipkech Lotiatia, amewataka wazazi kuhakikisha kwamba wanaweka mazingira bora na yenye utulivu kwa wanafunzi wanaotarajiwa kufanya mitihani ya kitaifa ya KCSE na KPSEA mwaka huu. Bw. Lotiatia alisisitiza umuhimu wa kuwapa watahiniwa hao usaidizi wa kila aina ili kuwawezesha kufanya mitihani yao bila kukumbwa na changamoto yoyote.

Aliongeza kuwa maafisa wa usalama wamejipanga kikamilifu kuhakikisha usalama wa kutosha wakati wote wa mitihani, ili kuzuia hali yoyote itakayovuruga utaratibu. Vilevile, aliweka wazi kwamba vitendo vya udanganyifu havitavumiliwa kamwe, akitoa onyo kali kwa wale wanaopanga kujihusisha na udanganyifu wa aina yoyote. Kamishna huyo alieleza kwamba watashirikiana na asasi zote husika kuhakikisha kuwa yeyote atakayepatikana akivuruga mitihani anachukuliwa hatua kali za kisheria.

Kamishna Lotiatia pia aliwataka wazazi kuwahimiza watoto wao kuwa watulivu na kuzingatia mitihani huku wakiwa na hakika ya usalama wao, akisema juhudi zote zimewekwa kuhakikisha mitihani hiyo inafanyika bila matatizo yoyote.

Mitihani ya kitaifa iling’oa nanga jana kwa wanafunzi wa kidato cha nne, huku wale wa gredi ya sita wakitarajiwa kuanza mitihani yao juma lijalo. Zaidi ya watahiniwa laki 9 wanafanya mtihani wa KCSE mwaka huu kote nchini.

October 23, 2024

Leave a Comment