Askofu wa jimbo katoliki la Ngong na ambaye pia ni mwenyekiti wa kitaifa wa tume ya Amani na haki katika Kanisa katoliki askofu John Oballa Owaa,hii leo amezindua rasmi kampeni ya kwaresma itakayoendelea kwa siku arubaini kuanzia tarehe 14 mwezi huu.

Akizungumza katika jimbo katoliki la Embu ambako uzinduzi huo ulifanyika, Askofu Oballa amewatolea mwito wakristu kutunza mazingira kwa kupanda miti akisema kuwa hiyo pia ni njia moja ya kuzingatia Amani na haki.

Wakati huo huo maaskofu pamoja na mapadri wa kanisa katoliki kutoka majimbo yote nchini, leo waliungana kwenye ibada ya misa takatifu katika kathedrali ya watakatifu Petero na Paulo katika jimbo katoliki la Embu kwa uzinduzi rasmi wa kampeni ya Kwaresma.

Askofu wa jimbo kuu la Nyeri askofu mkuu Anthony Muheria, ametoa himizo kwa wakristu kote nchini kuzingatia uadilifu kwa kila jambo wanalofanya msimu huu wa kwaresma.

Kwa upande wake mkurugenzi wa kituo hiki cha Radio Osotua Padri Francis Mwangi aliyehudhuria misa hiyo, amewashauri wakristu kujinyima na kunyenyekea msimu wa kwaresma. Kauli mbiu ya mwaka huu ni Uadilifu kwa Taifa yenye haki.

February 9, 2024