Kiongozi wa muungano wa Azimio La Umoja One Kenya Raila Odinga Jumatatu alasiri alijitokeza katika eneo la Kawangware jijini Nairobi kuanzisha maandamano ya pili dhidi ya serikali.
Odinga alikuwa ameandamana na kinara mwenza Martha Karua, kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka na kiongozi wa Roots Party George Wajackoyah, miongoni mwa viongozi wengine wa upinzani.
Dakika chache baada ya maandamano hayo kuanza ambapo msafara wa Odinga ulikuwa ukipita katika eneo la makazi, polisi waliwarushia vitoa machozi waandamanaji waliokuwa wamebeba matawi, mabango, vyombo na baadhi ya vyakula kuashiria gharama ya juu ya maisha.
Wakati huohuo Kampuni ya East Africa Specter Limited, inayomilikiwa na kiongozi wa Azimio, Raila Odinga, ilishambuliwa hii leo baada ya watu wasiojulikana kupiga mawe sehemu ya mali hiyo.
Katika video zilizochapishwa kwenye mtandao wa kijamii,madirisha kadhaa yalivunjwa na mawe yaliyotapakaa kwenye lango la jumba hilo.
Kanda nyingine ya CCTV inaonyesha idadi ya watu takriban 20 wakirusha mawe nje ya lango.
Meneja wa ulinzi na usalama katika kampuni hiyo Humphrey Waswa amesema kuwa watu hao walifika eneo hilo wakiwa na pikipiki na kuanza kurusha mawe kwa takriban dakika 30 kabla ya maafisa wa polisi kufika na kuwatawanya watu hao.
Uchunguzi zaidi kuhusu suala hilo unaendelea.