Rais William Ruto ametetea mpango wa mafuta kati ya Serikali za Kenya, Saudi Arabia na UAE akisema uliendeshwa kwa uwazi. Kwa mujibu wa rais Ruto ni kwamba mpango huo ulikuwa muhimu katika kupunguza shinikizo la Dola huku akidai kuwa ukosefu wa sarafu hiyo ulisababisha uhaba wa mafuta nchini.
Rais alieleza kuwa Serikali si dalali katika mpango huo bali ni mdhamini tu wa makampuni ya kimataifa ya mafuta kusambaza bidhaa hiyo muhimu kwa miezi sita kwa mkopo.
Wakati huo huo Kampuni tatu zinazotuhumiwa kwa ukiukaji wa sheria katika mkataba wa mafuta zimetoa taarifa ya pamoja na kukanusha madai kuwa zinatumiwa kupandisha bei ya mafuta nchini.
Katika taarifa hiyo ya pamoja, kampuni za Gulf Energy, Galana Energies na Oryx Energies zilikanusha madai kwamba hakukuwa na mkataba wa makubaliano uliotiwa saini katika mkataba wa mafuta kati ya serikali hizo tatu.
Hali kadhalika Kampuni hizo zilitupilia mbali madai kwamba zimeondolewa kulipa ushuru wa asilimia 30 wa kampuni zikisema kama mashirika mengine yote, yamekuwa yakilipa kodi zote zinazohusika.