Mshukiwa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda, Fulgence Kayishema, amekamatwa nchini Afrika Kusini. Haya yamesemwa Alhamisi na kitengo cha Umoja wa Mataifa cha kuchunguza uhalifu wa kivita uliofanywa nchini Rwanda.
Kulingana na kitengo hicho Kayishema anatuhumiwa kupanga mauaji ya karibu Watutsi elfu 2 wengi wao wakiwa watoto na wanawake waliokuwa wamepata hifadhi katika Kanisa Katoliki la Nyange wakati wa mauaji hayo ya kimbari ya mwaka 1994. Tangu mwaka 2001, Kayishema alitoweka na alikuwa hajulikani alipo. Taarifa zinasema mamlaka za Afrika Kusini zilisaidia katika kukamatwa kwa polisi huyo wa zamani wa mahakama.
Kayishema anakabiliwa na mashitaka ya kufanya mauaji ya kimbari, kula njama ya kufanya mauaji ya kimbari pamoja na uhalifu dhidi ya ubinadamu. Mshukiwa huyo aliyezaliwa mwaka 1961, amekuwa akijificha tangu Julai 2001.
Watu zaidi ya 800,000 waliuawa kinyama katika muda wa siku 100 nchini Rwanda mwaka 1994, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya Watutsi. Wauwaji walikuwa Wahutu wenye misimamo mikali ya ukabila.