Kenya Airways

Shirika la usafiri wa ndege la Kenya Airways limetangaza kuwa litaanza tena safari zake za moja kwa moja kuelekea Luanda, Angola, kuanzia mwezi Machi mwaka huu. Tangazo hili limefuatia makubaliano ya pande mbili kati ya Rais William Ruto wa Kenya na Rais João Lourenço wa Angola, wakati wa mkutano wao uliofanyika jana katika ikulu ya Angola, mjini Luanda.

Katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano huo, Angola imeeleza kuwa imeanza mchakato wa kuondoa hitaji la visa kwa wasafiri wa Kenya, hatua ambayo inalenga kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi kati ya mataifa haya mawili. Rais Ruto alitaja kwamba hatua hii ni muhimu kwa kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kutoa fursa kwa wataalamu wa Kenya kama walimu na wahandisi kufikia Angola kwa urahisi zaidi.

Aidha, Rais Ruto alitumia ziara hiyo kumpigia debe aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga, katika azma yake ya kuwania nafasi ya mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AU) katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao. Rais Ruto alisisitiza kuwa Odinga ana uwezo wa kuongoza AU kutokana na uzoefu wake wa muda mrefu katika siasa za kimataifa.

January 9, 2025

Leave a Comment