Mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwah ndiye Kiongozi mpya wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, baada ya spika wa bunge hilo Moses Wetangula kutoa uamuzi kuhusu mrengo ulio na wawakilishi wengi bungeni. Katika uamuzi wake Alhamisi 06, Oktoba 2022, spika Wetangula aliweka bayana kuwa mrengo wa Kenya kwanza una wabunge 179 dhidi ya wabunge 157 walio katika mrengo wa Azimio la Umoja.
Bunge lililazimika kusubiri uamuzi wa Spika kuhusu suala mrengo unaaongoza kwa idadi kabla ya kuanza kwa shughuli zake rasmi, baada ya vuta nikuvute kutoka kwa mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio la Umoja One Kenya Alliance ambayo ilidai kuwa na idadi ya juu zaidi ya wawakilishi bungeni. Kutokana na uamuzi wa leo, spika pia amemuidhinisha Mbunge wa Kilifi Kaskazini Owen Baya kuwa naibu wa kiongozi wa wengi bungeni. Katika wadhifa mwingine wa uongozi wa bunge hilo, Mbunge wa Mugirango Kusini Sylvanus Osoro atakuwa Mnadhimu Mkuu, akisaidiwa na Mwakilishi wa Kike wa kaunti ya Marsabit Naomi Waqo.
Uamuzi wa Spika Wetangula pia unamaanisha kuwa muungano wa Azimio La Umoja One Kenya ndio muungano wa wachache katika Bunge hilo, na hivyo kutwaa nyadhifa za walio wachache. Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi atakuwa Kiongozi wa Wachache, akisaidiwa na Mbunge wa Kathiani Robert Mbui, huku Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed akiwa mnadhimu wa walio wachache akisaidiwa na Mbunge Mteule Sabina Chege.
Vikao hivyo vya bunge alasiri ya leo vilikatizwa kabla ya kukamilika, kutokana na vurugu na mvutano katika vikao hivyo, wabunge wa mirengo tofauti wakizozana baada ya kutangazwa kwa viongozi wa wengi na wachache katika bunge. Spika Moses Wetangula alitangaza kusitishwa kwa vikao hivyo na kuwataka wabunge kukongamana tena Jumanne ya tarehe 11 Oktoba 2022, saa nane unusu adhuhuri kwa vikao vingine vya bunge hilo la 13.